Tuesday, 17 January 2017

Shule ya Msingi ya Serikali ya Kijijini Inayong'ara katika Mitihani ya Kitaifa

Wiki hii serikali ya Tanzania ilitangaza matokeo ya mitihani ya kupima wanafunzi wa kidato cha pili na darasa la nne kwa mwaka 2016. Mengi yamezungumzwa katika mitihani hiyo, hasa habari ya shule za binafsi kung'ara katika matokeo hayo na shule za serikali kushika mkia.

Lakini kuna jambo la kipekee katika matokeo hayo. Jambo hili linahusu shule ya msingi Majulai, ambayo pamoja na kuwepo kijijini sana wilayani Lushoto mkoani Tanga katika tarafa ya Mlalo, kata ya Mwangoi, shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri sana katika mitihani mbalimbali ya shule za msingi. 


Pamoja na kuwepo katika mazingira ya kijijini, shule hiyo imeonekana kushindana na shule nyingi zilizoko mazingira ya mjini ambako kuna walimu wa kutosha na vifaa vingi vya kufundishia. Mfano, katika mtihani wa darasa la nne mwaka 2016 shule hiyo imeshika nafasi ya pili (2) katika wilaya ya Lushoto kati ya shule 129 na kushika nafasi ya 4 katika mkoa wa Tanga kati ya shule 601. Shule hiyo ya serikali ya kawaida kabisa kama zilivyo shule nyingine za serikali imeshika nafasi ya 43 kitaifa kati ya shule 11,025, nafasi ambayo haijaweza kufikiwa hata na shule nyingi za binafsi ambazo wazazi hulipia pesa nyingi sana kuhakikisha watoto wao wanapata elimu nzuri.

Je, kuna kitu gani katika shule hii ambacho kinaweza kutoa funzo kwa shule nyingi hasa zile za serikali ambazo zimeendelea kubaki nyuma katika matokeo?. Kuna haja ya kujifunza kutoka shule hiyo. 


TAZAMA MATOKEO YA SHULE YA MAJULAI HAPA.

No comments: