Tuesday 25 March 2014

BMU Zasaidia Huduma za Jamii Mafia

Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Raslimali za Uvuvi (BMUs) vimeanzishwa na serikali kwa lengo kuu la kuishirikisha jamii ya wavuvi katika suala zima la kusimamia raslimali za uvuvi, ili ziweze kutumika kwa busara na kuleta matumizi endelevu ya raslimali hizo. Hii inafanywa na jamii kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile serikali kuu, serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Kwa mujibu wa Mwongzo wa Uanzishwaji wa Vikundi vya  Usimamizi Shirikishi wa  Raslimali za Uvuvi wa Kitaifa, BMUs zinazotumia eneo fulani katika uvuvi zinaweza kuungana na kuanzisha  Maeneo ya Usimamizi wa  Pamoja (CFMA) katika  Ukanda wa Bahari ya Hindi.

“Sababu kuu ya kuanzishwa  maeneo ya usimamizi wa pamoja wa uvuvi ni kutambua haki za vijiji jirani, za kutumia raslimali zilizopo ndani ya eneo na hivyo kusimamia kwa pamoja raslimali hizo”, kwa mujibu wa Mwongozo huo.


Wana BMU wa B weni, Mafia wakipanga Mpango Mkakati wa BMU yao
Usimamizi shirikishi unatambuliwa pia na sheria ya uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni za uvuvi za mwaka 2009  ambapo mamlaka yanatolewa kwa jamii ya wavuvi kuanzisha Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Raslimali za Uvuvi (BMUs), unaolenga kuzipa uwezo jamii za wavuvi majukumu ya usimamizi wa raslimali za uvuvi kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine, kukuza uboresheaji wa makazi ya viumbe yaliyoharibiwa pamoja na kuongeza wingi wa viumbe wa bahari waliohatarini kutoweka kwa kupunguza nguvu ya uvuvi hasa uvuvi haramu usiozingatia sheria na shughuli haribifu za mazingira.

Pia kusaidia na kukuza ufuatiliaji, tathmini na utafiti wa raslimali za uvuvi ili kuwezesha kutoa msingi wa maamuzi sahihi ya usimamizi na kukuza mwamko kuhusu masuala ya usimamizi endelevu wa raslimali za uvuvi katika maeneo ya jamii.

Akizungumzia usimamizi shirikishi katika warsha ya uzinduzi wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Raslimali za Uvuvi unaotekelezwa na WWF Tanzania na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na WWF Uingereza (WWF-UK), Naibu Mkurugenzi wa Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi Tanzania, Fatma Sobo alisema, “Nia na lengo la wadau wote katika usimamizi shirikishi ni kuwa na uvuvi endelevu, uvuvi ambao utaturuhusu tuvue sisi, vizazi vyetu na vizazi vijavyo”. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uvuvi wa wizara hiyo katika hotuba ya kufunga warsha iliyofanyika mjini Dar es Salaam Mei 17, 2013, Bi. Sobo aliongeza “Kama wenzetu waliopita waliweza kutunza raslimali zetu, nasi tunapaswa kuzitunza pia”.

Alisema wizara yake itashirikiana na wadau wote muhimu katika kutekeleza mradi huo muhimu unaotekeleza kile kilichopo katika sera ya uvuvi ya mwaka 1997 na sheria ya mwaka 2003.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania,
Maria Iarrera
alisema Umoja wa Ulaya unatambua umuhimu wa wananchi kushirikishwa katika kusimamia raslimali zao wenyewe. 

“Ni muhimu wanajamii kuelewa kuwa usimamizi shirikishi ndiyo njia pekee itakayoleta maendeleo endelevu ya raslimali na kwamba wana jamii wanaweza kufaidika na usimamizi huo kwa raslimali kuongezeka,” alisema, na kuongeza kuwa ana matumaini kuwa mradi huo utazidi kufikia watu wengi zaidi katika ukanda wa pwani.

Pamoja na usimamizi wa raslimali za uvuvi, kuanzishwa kwa vikundi vya BMUs katika Kisiwa cha Mafia kumeonyesha matunda zaidi ya usimamizi wa raslimali hizo. Vikundi hivyo vimeanza sasa kuchangia katika shughuli za maendeleo ya jamii kama vile ujenzi wa zahanati, usafi wa mazingira na ujenzi wa madarasa ya shule.

“BMU yetu imeshiriki kuchangia fedha taslimu kwa ajili ya kusafisha mto. Lengo la kusafisha mto huo ni kuimarisha usafi katika eneo la mwalo,” anasema mwenyekiti wa BMU ya Kilindoni, Kassim A. Ahmadi.

Kwa mujibu wa Ahmadi, mbali na BMU kutoa huduma ya kusafisha mto, pia imechangia katika gharama za ujenzi wa zahanati, kutoa mafunzo ya usimamizi shirikishi kwa viongozi wapya wa BMU na pia kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia kufanya doria katika eneo lililopo chini ya usimamizi wao. Jumla ya Shs. 700,000 zimetumika katika huduma hizi.

“Mchango wetu kwa jamii unatambulika na serikali ya kijiji,” anasema mwenyekiti huyo. “Hata sasa kuna barua hii ambapo serikali ya kijiji imetutaka BMU kuchangia Shs. 500,000 katika mpango wa kutoa chakula kwa shule zetu za msingi,” anasema huku akionyesha barua ya maombi ya mchango kutoka serikali ya kijiji chake.

BMUs nyingine zinazokiri kuchangia katika shughuli za maendeleo ya jamii ni pamoja na Chunguruma na Ndagoni. Wakati Chunguruma wanakiri kuchangia katika ujenzi wa nyumba ya mkunga katika zahanati ya kijiji, Ndagoni wanakiri kuwahi kutoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya sekondari.

BMUs zote hizo hapo juu zilianzishwa na shirika la WWF Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, Idara ya Uvuvi na Mradi wa MACEMP chini ya Programu yake ya  Rufiji, Mafia na Kilwa (RUMAKI) iliyoanza mwaka 2005 hadi 2012. Chini ya programu hiyo, BMUs 25 zilianzishwa katika wilaya hizo tatu.

Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Raslimali za Uvuvi  una lengo la kuendelea kuziimarisha BMUs zilizopo na kuanzisha BMUs nyingine 67 kuanzia mwaka 2013 hadi mradi utakapohitimishwa mwaka 2017. BMUs hizi zitaanzishwa katika wilaya tano za Rufiji, Mafia, Kilwa, Mtwara Vijijini na Manispaa ya Temeke.

Pia mradi utaendelea kufuatilia na kuzijengea uwezo BMUs zilizoundwa wakati wa RUMAKI na zitakazoundwa kwa sasa ili kuwa na ufanisi zaidi katika utendaji wake wa kazi.

“Lengo kubwa la BMUs ni kusimamia raslimali za uvuvi na pwani,” anasema Paul Kugopya, Afisa wa Usimamizi Shirikishi wa Mradi huo katika wilaya ya Mafia. “Lakini BMUs zitafikia  malengo ya kusimamia raslimali za uvuvi pale tu zitakapoonyesha uwezo wa kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa raslimali kwa kuzuia uvuvi haramu, hivyo kuongeza kipato cha jamii kupitia uvuvi na kutatua tatizo sugu la umaskini unaoikabili jamii ya  Watanzaia na kuwa na uwezo wa kutosha wa kusaidia huduma na shughuli za kijamii katika vijiji vyao kwa kushirikiana na Halmashauri za vijiji”.

No comments: