Wednesday 26 March 2014

Utafiti wa Potwe Wataka Usimamizi Bora wa Utalii Kisiwani Mafia


Utafiti wa potwe unaoendelea kisiwani Mafia kwa ufadhili wa WWF Tanzania unapendekeza kuboreshwa kwa usimamizi wa utalii kwa kuandaa mpango wa usimamizi na maendeleo ya utalii.  



Potwe akiwa amezungukwa na samaki - Picha na Mtafiti wa Potwe
Clare Prebble


Utafiti wa awali kuanzia mwaka 2007 hadi 2009 uliofanywa na WWF kwa kushirikiana na Taasisi ya Potwe ya Marekani ulikuwa na lengo la kujua idadi ya potwe katika kisiwa cha Mafia. Utafiti uligundua kuwa kati ya potwe 40 hadi 50 walikuwa wakiishi Mafia na kila mmoja alikuwa na madoa maalum mwilini mwake ambayo yaliweza kumbainisha. Utafiti pia ulibaini kuwa karibu potwe wote walioishi kisiwani humo walikuwa wenye umri mdogo na walikuwa wa jinsi ya kiume. Pia wengi walionekana kila mwaka kati ya mwezi Aprili na  Oktoba.

Utafiti wa karibuni wenye jina la “Sababu za Kimazingira Zinazoathiri Kuwepo kwa Potwe na Mwenendo Wake Kisiwani Mafia, Tanzania”,  ambao ulipanua wigo wa utafiti wa awali, miongoni mwa mambo mengine, ulitaka kujua hali ya kimazingira ya bahari katika ukanda, mfumo wa idadi ya potwe, mwenendo wake, tabia za ulaji, mwingiliano na wavuvi na tishio la kibinadamu dhidi ya potwe katika kisiwa cha Mafia.

Ikilinaganishwa na utafiti wa awali, matokeo ya utafiti wa wakati huu uliofanywa na shirika la “Marine Mega Fauna Foundation”, Chuo cha Mfalme Abdullah cha Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania kati ya mwezi Oktoba 2012 na Machi 2013 umegundua kuwepo kwa  potwe wa aina mbalimbali 87.

“Utafiti pia umegundua kuwa potwe wanapatikana kisiwani Mafia hata kama wasipoonekana katika maji ya juu kwani muda wa kuishi kisiwani ni siku 75 ikilinganishwa na siku 40 kwa mwaka katika mahali pengine kwenye Bahari ya Hidi na wanarejea Mafia kila mwaka,” anasema Jason Rubens, Mshauri Mtaalam na mratibu wa zamani wa Programu ya Bahari ya WWF. “Kwa hiyo utafiti umeshaonyesha kuwa kisiwa cha Mafia ni cha kipekee kwa maisha ya potwe”.

Utafiti mwingine unaoendelea kwa sasa ni kujua ni kwa nini potwe wanapenda kuja kuishi Mafia. “Mafia inajulikana kutokana na kuwa na chakula kingi kwa ajili ya potwe, lakini utafiti unahitaji kubainisha kama kweli wanakuja kwa ajili ya chakula, hali ya chakula maeneo mengine ya Bahari ya Hindi ikoje,” Rubens anasema.


Utafiti pia utasaidia kubainisha kama kuna hali ya kipekee ya mazingira ya kuzaliana potwe katika eneo la Rufiji, Mafia na Kilwa (RUMAKI). Inajulikana kuwa hili ni eneo linalopata virutubisho vingi kutoka Mto Rufiji. Ugunduzi huu unaweza kuhusishwa na suala zima la umuhimu wa kuundwa kwa Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Mazingira ya Bahari na Pwani (BMUs) ili kuhifadhi rasilimali za majini na samaki na mazingira yote ya ukanda wa RUMAKI, kwa mujibu wa Rubens.

Pia utafiti unaweza kuelezea ni kwa nini uvuvi wa samaki aina ya dagaa unaendelea kushamiri katika kisiwa cha Mafia. Pengine ni kutokana na urahisi wa upatikanaji wa chakula katika ukanda huo ambacho pia kinaliwa na potwe.

Katika suala la utalii, kuna wito umetolewa na utafiti uliopita juu ya umuhimu wa kuwepo kwa Mpango wa Kusimamia Utalii wa Potwe Mafia. “Utalii usiosimamiwa vizuri unaweza kufukuza potwe kutoka kisiwa cha Mafia kutokana na uwezekano wa watalii kubughudhi tabia za potwe hasa katika ulaji wao,” Rubens anasema. “Kama utalii usiposimamiwa vizuri unaweza kuwa na athari mbaya”, anasisitiza akitoa mfano wa yaliyojitokeza katika utalii wa pomboo huko Zanzibar ambapo watalii walikuwa wakiongezeka bila kuwepo kwa mpango maalum wa kusimamia utalii huo.

Anasema hali ya sasa inaonyesha kuwa hadi boti 7 zinaweza kuingia kupeleka watalii kuogelea na potwe na baadhi ya watalii wameshaanza kulalamikia hali hiyo. Anasema kwa kuwa na mpango wa usimamizi, itawezesha kuzuia idadi ya boti zinazoingia kupeleka watalii kuogelea na potwe kwa sababu zitaingia baharini kwa kufuata utaratibu uliokubalika.

Maoni yake yanaungwa mkono na utafiti. Kwa mujibu wa utafiti wa potwe, viumbe hao katika kisiwa cha Mafia wanakabiliwa na athari za kimazingira ambazo zinaweza kuathiri maisha yao au tabia zao. “Idadi kubwa ya potwe (asilimia 75%) wana makovu na pamoja na kwamba makovu mengi ni madogo madogo, hii inaonyesha wazi kuwa suala la mgongano na boti ni la kawaida,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni.

Inaongeza kuwa makovu yamewapata potwe katika kisiwa cha Mafia zaidi ikilinganishwa na mahali pengine katika Bahari ya Hindi mfano Shelisheli (67%), Msumbiji (37%) na Australia (27%).

Ripoti inasema kuwa michirizi inayoonekana mgongoni inawezekana ilitokana na kugongana na boti. Makovu mengi pia yanaonekana kusababishwa na boti ndogo ndogo kama vile boti za watalii ambazo zinajishughulisha na kuangalia potwe na pia boti za wavuvi wa dagaa.
 

“Kuna haja kwa serikali ya wilaya kutengeneza mpango wa usimamizi wa utalii sasa na kukubaliana na wenye boti jinsi ya kusimamia utalii wa potwe,” anahitimisha Rubens.

No comments: